Jjuuko apewa mikoba ya Nyoni

*Beki huyo kiraka arejeshwa Dar kwa vipimo

*Vigogo Simba, serikalini wapata mshtuko

SAADA SALIM, ZANZIBAR

KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, ameanza kumwandaa beki wake, Jjuuko Murushid, kuchukua nafasi ya Erasto Nyoni, ambaye hatakuwepo katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura ya Algeria Jumamosi ya wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Nyoni ameondolewa katika mipango ya  kocha huyo katika mchezo huo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuumia goti wakati wa mechi ya juzi ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar dhidi ya KMKM, Uwanja wa Amaan, Unguja.

Kitendo cha kuumia kwa beki huyo kimewatia hofu viongozi wa Simba, wakiongozwa na Mtendaji Mkuu (CEO), Crescentius Magori, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Swed Mkwabi, aliyekuwa Rais wa Wekundu wa Msimbazi hao, Salim Abdallah `Try Again` na mashabiki walikuwepo uwanjani hapo wakishuhudia mchezo huo.

Licha ya hofu waliyopata viongozi hao wa Simba, lakini pia mmoja wa vigogo serikalini, ambaye naye ni shabiki mkubwa wa Simba, naye alimpigia simu mmoja wa viongozi wa klabu hiyo aliyepo visiwani hapa kutaka kufahamu juu ya maendeleo ya Nyoni baada ya kuumia.

Akizungumza na BINGWA jana, Aussems alisema kutokana na kuumia kwa beki wake huyo, hataweza kumtumia katika mchezo wao huo wa kimataifa na sasa kuhakikisha anamtengeneza Murushid kuchukua nafasi yake.

“Kwangu ule ushindi (dhidi ya KMKM) haukuwa na maana yoyote, kwani tayari akili yangu ilikuwa ikiwaza majeruhi ya Nyoni, kumkosa mechi ya Jumamosi.

“Kuna wachezaji wazuri ambao wataweza kuchukua majukumu ya Erasto, akiwamo Jjuuko ambaye amekuwa na uzoefu mkubwa wa michuano ya kimataifa kwa kucheza mara kwa mara katika timu yao ya Taifa,”alisema.

Aussems alisema anamwamini Murushid na anachokifanya kwa sasa ni kuhakikisha anawajenga wachezaji wake kisaikolojia na kila mmoja kufanyia kazi majukumu yake.

Alisema amefanikiwa kuangalia mikanda ya JS Saoura na kubaini wachezaji wao wako vizuri na kutumia nguvu zaidi, hasa katika safu ya ushambuliaji na mabeki.

“Nafanyia kazi madhaifu yao pamoja na kuongeza mbinu kwa vijana wangu, hasa katika safu ya ulinzi baada ya kuumia kwa Nyoni na huenda Jjuuko akawa mmojapo watakaobeba majukumu hayo ya kuwazuia Waalgeria,” alisema.

Habari za kuaminika zilizolifikia BINGWA jana zinasema kuwa baada ya kufanyiwa vipimo vya MRA, Nyoni ametakiwa kukaa nje kwa muda wa wiki tatu na tayari jana amerejea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Alipotafutwa daktari wa Simba, Yassin Gembe, kuzungumzia maendeleo ya nyota wao huyo, alisema hawezi kuwekawazi juu ya muda atakaokaa nje, kwani bado hajakabidhiwa vipimo alivyopimwa.

“Bado hatujapewa majibu ya vipimo, hizo habari za wiki tatu mmezitoa wapi? Baada ya kupokea taarifa kutoka hospitali, nitawafahamisha,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*