Jeshi la Yanga ‘full’ muziki leo

NA WINFRIDA MTOI

WACHEZAJI wa Yanga waliokuwa wanashiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar, leo wanatarajia kuungana na wenzao katika mazoezi yanayoendelea katika Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar es Salaam.

Kikosi cha Yanga kilitolewa katika hatua ya makundi ya mashindano hayo, baada ya kufungwa mechi mbili na kushinda mbili kati ya nne walizocheza.

Akizungumza na BINGWA jana, Mratibu wa timu ya Yanga, Hafidh Saleh, alisema wachezaji hao waliwasili juzi na kupewa mapumziko ya siku moja, hivyo leo wataungana na wengine kujiandaa na mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Alisema kwa sasa bado hawajapewa ratiba ya mechi yao dhidi ya Azam iliyoahirishwa kutokana na mashindano ya Kombe la Mapinduzi, hivyo wataendelea kujifua kwa ajili ya mzunguko wa pili.

Aidha, alisema Januari 16 mwaka huu wanatarajia kucheza na Mwadui FC katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kabla ya kuivaa Stand United.

“Leo (jana) waliokuwa wamebaki Dar es Salaam wamefanya mazoezi, lakini kesho (leo) wote wataungana kujiandaa na mechi zijazo za Ligi Kuu,” alisema Saleh.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*