HATUNA CHA KUPOTEZA


ZAITUNI KIBWANA NA HUSSEIN OMAR

KIKOSI cha Simba kimepanga kuondoka keshokutwa kwenda mjini Lubumbashi, DR Congo kuwafuata TP Mazembe, huku Wekundu wa Msimbazi wakiahidi kuwashambulia wapinzani wao hao mwanzo mwisho kwani hawana la kupoteza.

Timu hizo zitakutana Jumamosi hii katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa ni baada ya juzi kutoka suluhu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pamoja na matokeo hayo ya uwanja wa nyumbani, Simba inaamini ina uwezo wa kusonga mbele, ikitamba kufanya kweli ikiwa ugenini DR Congo.

Kati ya mbinu walizopanga Simba kuzitumia watakapokutana na wapinzani wao hao kwenye Uwanja wa Stade TP Mazembe unaomilikiwa na mabingwa hao wa Afrika mara tano, ni kupanga washambuliaji wao wote watatu, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na nahodha wao, John Bocco.

Nyuma yao kutakuwa na viungo matata, Haruna Niyonzima, Clatous Chama, Jonas Mkude na James Kotei watakaokuwa na kazi ya kusaidia ulinzi na kuwalisha straika wao.

Nao mabeki wa pembeni, Zana Coulibaly wa kulia na Mohammed Hussein (kushoto), pamoja na kulilinda lango, watatumika zaidi kupandisha mashambulizi na kupiga krosi zitakazowakosesha amani mabeki na viungo wa TP Mazembe.

Ni kwa kufanya hivyo, Simba wanaamini wanaweza kuwapa presha wapinzani wao na kujikuta wakichanganyikiwa na kuwafunga kirahisi.

Akizungumza na BINGWA jana, Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi, alisema wameshatanguliza watu wa kazi DR Congo kwa ajili kuandaa mazingira timu itakapofikia, hoteli na uwanja wa kufanyia mazoezi.

“Kila kitu kipo sawa na kimsingi tumepanga kwenda kufanya maajabu kule ndio maana hata mikakati yetu tunataka iwe siri,” alisema Mkwabi.

Aliongeza: “Hatujakaa, hatujalala… tunataka kufanya maajabu, mashabiki wetu waelewe tupo tunapambana, tunataka kwenda nusu fainali Ligi ya Mabingwa ili tuweke historia.”

Mkwabi alisema kwa kutambua ugumu wa mchezo huo, wameomba Shirikisho la Soka Tanzania kuahirisha mchezo wao wa kesho wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Biashara United.

“Hatutacheza hiyo mechi kwa sababu tuna maandalizi, tumewaomba TFF na wametukubalia, hivyo hakuna tena huo mchezo ambao sisi ndio tulikuwa wenyeji,” alisema.

Kwa upande wake, Kocha wa Simba, Patrick Aussems, amesema amejipanga kuwavaa TP Mazembe kivingine kwa kushambulia tangu mwanzo wa mchezo ili kusaka mabao ya mapema yatakayowachanganya wapinzani wao.

Licha ya Simba kupewa nafasi ndogo ya kufanya vizuri katika mchezo huo wakiwa ugenini, lakini Aussems amesisitiza lolote linawezekana katika mchezo huo.

“Kwa kuongeza umakini zaidi, nina uhakika tunaweza kufunga na nina uhakika tunaweza kufuzu hatua inayofuata, tulikuwa na mchezo mzuri (juzi) na ninatarajia mchezo mzuri zaidi tukienda DR Congo,” alisema Aussems.

Kocha huyo kipenzi cha mashabiki wa Simba, aliongeza: “Tunafahamu kuwa tunahitaji kupata ushindi mzuri ili tuweze kufuzu, tutapambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri, kwani tunao wachezaji wa kutuwezesha kupata mabao ya mapema kama Kagere, Okwi, Bocco na Chama, bila shaka wote wataanza.”

Akiuzungumzia mchezo wa juzi, alisema anaamini bahati haikuwa kwao kwani walitengeneza nafasi nyingi za kufunga, ikiwamo penalti waliyopata lakini walishindwa kuzitumia.

“Naamini hata hao TP Mazembe watatukaribisha kwao wakiwa wanatuheshimu, waliona kilichotokea jana, tulicheza vizuri na tulistahili ushindi,” alisisitiza.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*