Djuma awapa neno Simba

NA ZAINAB IDDY

ALIYEKUWA kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, amewaambia Wekundu hao wa Msimbazi kuwa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura ya nchini Algeria, ni mgumu na unahitaji umakini kwani lolote linaweza kutokea.

Mchezo huo wa kwanza wa Kundi D  unatarajiwa kuchezwa leo katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na BINGWA kutoka nchini Rwanda, Djuma alisema wapinzani wa Simba ni wazuri hivyo wanatakiwa kuwa makini kwa kila nafasi watakayopata.

“Siku zote Waarabu wanafahamika ni wazuri na kama wakipata nafasi tatu ni lazima moja wataitumia vizuri, hivyo Simba watapaswa kujua hilo.

“Simba wakiruhusu nafasi za wazi kwa wapinzani wao ni hatari kwao, lakini pia ni muhimu wapate ushindi katika mchezo huu kabla ya kukutana na timu nyingine bora zaidi ya JS Saoura,” alisema Djuma.

Hata hivyo, alieleza kuwa anaamini Simba wanaweza kushinda mechi ya leo lakini wakikosa umakini wanaweza kufungwa mabao mengi.

“Bila shaka benchi la ufundi la Simba litakuwa limeshajua mbinu zote za JS Saoura na kuzifanyia kazi mapema,” aliongeza.

Mbali na Simba na JS Saoura, Kundi D lina timu nyingine za AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo (DRC) na Al Ahly ya nchini Misri.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*