Dante amvuruga Amunike

NA ZAINAB IDDY

KITENDO cha beki wa kati, Andrew Vicent ‘Dante’, kutokuwa fiti kimeonekana kumvuruga kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Emmanuel Amunike, kwani hadi sasa hajajua nani atakuwa mbadala wake.

Dante ni miongoni mwa mabeki walioitwa katika kikosi cha Stars kilichotangazwa kuivaa Uganda katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Uganda, utakaochezwa Machi 24, mwaka huu ndani ya dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Daktari wa Yanga, Edward Bavu, beki huyo anasumbuliwa na misuli, tangu walipocheza mchezo wa Azam Federation Cup dhidi ya Namungo FC, jambo lililosababisha kuwa nje ya kikosi hadi pale atakapokuwa fiti.

Akizungumza na BINGWA jana, Amunike, alisema taarifa za kuwa Dante ni majeruhi zimemchanganya kwani alikuwa na mipango naye katika mchezo wa Stars na Uganda.

“Siku bado na naweza kutafuta mbadala wake lakini taarifa za kutokuwa fiti kwa Dante zilipoletwa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) na timu yake zilinichanganya na sasa naumiza kichwa kuangalia nani atachukua nafasi yake.

“Kwa kuwa kambi inaanza Jumatatu, inabidi niangalie namna ya kufanya maamuzi sahihi haraka kabla ya mchezo huo ambao ni muhimu kwa Stars na ni lazima tushinde ili tucheze Afcon kule Misri,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*