CRISTIANO RONALD Kipenzi cha warembo mwenye tamaa ya mafanikio makubwa

TURIN, Italia

JUMANNE ya wiki hii, Juventus walifuta ndoto za Atletico Madrid kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Atletico waliiaga michuano hiyo baada ya kuchapwa mabao 3-0 katika mchezo wa marudiano, uliochezwa Hispania kwenye Uwanja wa Allianz.

Ronaldo ambaye hakufunga bao lolote kwenye mchezo wa kwanza ambao ulimalizika kwa Juventus kuchapwa mabao 2-0, aliimaliza kazi hiyo kwa kutupia ‘hat trick’ nchini Italia dhidi ya wapinzani wake wa zamani.

Mabao yake matatu yaliiwezesha mabingwa hao wa Italia kwenda robo fainali kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-0.

‘Hat trick’ hiyo imemfanya Ronaldo kuwa mwanasoka pekee aliyehusika kwenye mabao 77 ya hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Lakini pia, ilikuwa ni ‘hat trick’ yake ya nane sawa na Lionel Messi kwenye michuano hiyo.

Hebu cheki mambo haya ambayo huenda huyajui kuhusu staa huyo ambaye ni nahodha wa timu ya Taifa ya Ureno.

1.Anaitwa Cristiano Ronaldo dos Santos Aveiro. Mwanasoka huyo alizaliwa Februari 5, 1985 mjini Madeira, Ureno.

2.Jina la Ronaldo linatokana na aliyekuwa Rais wa Marekani, Ronald Reagan. Baba yake alimpachika jina hilo kwa sababu alikuwa kipenzi cha mwanasiasa huyo.

3.Kuna siri kubwa ya Ronaldo kutokunywa pombe. Ilikuwa hivi, baba yake, Jose Dinis Aveiro, alikuwa mlevi na alifariki dunia kwa tatizo hilo akiwa na umri wa miaka 52.

4.Ronaldo ni miongoni mwa wanasoka waliozaliwa katika familia masikini. Mama yake aitwaye Maria Dolores dos Santos Aveiro, alikuwa mpishi na baba yake alikuwa mtunza bustani.

5.Ronaldo alifukuzwa shule akiwa na umri wa miaka 14. Kosa lake lilikuwa ni kumrushia kiti mwalimu wake. Nyota huyo alisema aliamua kufanya hivyo kwa sababu mwalimu wake alimdharau.

6.Mshikaji huyo anatajwa kuwa na utajiri wa Dola za Marekani milioni 250. Kiasi hicho ni zaidi ya Sh milioni bilioni 550. Mwaka 2014 pekee, mshambuliaji huyo aliingiza Dola milioni 80.

7.Mwaka 2010, Ronaldo alipata mtoto wake wa kwanza aitwaye Cristiano Jr. Ilidaiwa kuwa alimlipa mwanamke mmoja ili akubali kupandikiziwa mbegu.

8.Ronaldo si aina ya mastaa wanaopendelea kuipamba miili yao kwa ‘tattoo’. Sababu kubwa ya nyota huyo kutochora michoro hiyo ni kwa kuwa amekuwa akichangia damu mara kwa mara.

9.Unamjua mwigizaji Arnold Schwarzenegger? Mkali huyo wa filamu za mapigano ni shabiki mkubwa wa Ronaldo.

10.Jamaa huyo huwezi kumweka kando linapokuja suala la kuwanyatia warembo. Kwa nyakati tofauti, aliwahi kutoka na mastaa Paris Hilton (2009), Kim Kardashian (2010) na Irina Shayk (2011).


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*