Bocco aongeza mwaka Simba

TIMA SIKILO

HATIMAYE mshambuliaji wa Simba, John Bocco, ameongeza mkataba wa mwaka mmoja zaidi Simba na hivyo kuzima tetesi za kuhusishwa na klabu yake ya zamani ya Azam iliyokuwa imepanga kumrejesha Chamazi, Dar es Salaam.

Habari zilizonaswa na BINGWA jana kutoka kwa mmoja wa vigogo wa Simba, zinasema kuwa Bocco ni miongoni mwa wachezaji ambao klabu hiyo haikuwa tayari kuwapoteza kutokana na mchango wake Msimbazi.

“Bocco tayari ameshaongeza mkataba wake wa mwaka mmoja zaidi. Ni mchezaji aliyetoa mchango mkubwa sana Simba akiwa kama kiongozi wa wenzake na mchezaji pia.

“Akiwa kama nahodha wa timu, ametekeleza majukumu yake ipsavyo lakini kama mchezaji, ametoa mchango mkubwa kuiwezesha timu kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na sasa tukiwa katika nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Mchezaji kama huyo huwezi kumwacha kirahisi,” alisema kigogo huyo.

Katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Bocco alitoa mchango mkubwa mno, akifunga mabao muhimu na kutoa pasi za mabao, huku hadi jana akiwa amecheka na nyavu mara 15 Ligi Kuu Bara na kuchangia mengine lukuki.

Mbali ya Bocco, kigogo huyo mwenye ushawishi wa aina yake Simba, alisema kuwa wapo katika mchakato wa kumalizana na kiungo wao, Jonas Mkude kabla ya kuwageukia wengineo.

Hadi sasa, Simba ipo kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa na pointi 88 baada ya kushuka dimbani mara 35, ikiwa imebakiza mechi tatu tu kuhitimisha ligi hiyo inayofikia tamati mwishoni mwa wiki hii.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*