Beki Yanga awatangazia vita Msimbazi


WINFRIDA MTOI

BEKI wa timu ya Yanga, Andrew Vicent ‘Dante’, ametangaza vita kwa mahasimu wao Simba akisema watakula nao sahani moja katika kupigania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Baada ya Yanga kupoteza mechi dhidi ya Mtibwa Sugar wakifungwa bao 1-0, Simba wapinzani wao wakubwa katika mbio za ubingwa nao walipunguzwa kasi na Kagera Sugar.

Akizungumza na BINGWA, Dante alisema wanafahamu wapinzani wao wana hasira ya kuondolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kitendo ambacho kinawafanya waelekeze nguvu zote Ligi Kuu.

Alisema Yanga inazungumziwa kwamba haipo kwenye ubora kutokana na kutofanya vizuri katika baadhi ya michezo, lakini ukweli uliopo hawajakata tamaa ya ubingwa hivyo watapambana hadi dakika ya mwisho.

“Simba wameondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na hasira zote wamehamishia Ligi Kuu wakilenga zaidi kutetea ubingwa wao, hivyo lazima watacheza mechi zao kwa kasi,” alisema Dante.

Dante aliongeza kuwa wakati Simba wanapambana wakumbuke kuwa Yanga pia wapo katika mapambano, hivyo kila mmoja atahesabu alichokivuna mwishoni mwa ligi.

“Sisi tumecheza mechi nyingi kuliko wao ila najua kuna sehemu tutawakamata, Simba hawawezi kushinda michezo yote ya viporo kwa sababu kipindi hiki mechi zote ni ngumu maana kila timu inahitaji matokeo ya ushindi,” alisema Dante.

Hata hivyo, beki huyo alikiri kwamba wanatambua wanakabiliwa na mechi ngumu na kila mmoja anakiangalia kikosi chao kwa jicho la tofauti, lakini amewataka wafahamu bado wapo katika mbio za ubingwa wakichuana na Wekundu wa Msimbazi.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Yanga inashika usukani ikiwa imevuna pointi 74 baada ya kucheza mechi 32 ambapo wameshinda 23, sare tano na kufungwa nne.

Kwa upande wa Simba wao wanashika nafasi ya tatu baada ya kujikusanyia pointi 60, wakiwa wameshuka dimbani mara 24 na kushinda 19, sare tatu na kufungwa mbili.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*