Basena aomba kazi Azam FC

NA TIMA SIKILO

KOCHA wa zamani wa timu ya Simba raia wa Uganda, Moses Basena, ni miongoni mwa makocha walioomba kazi ya kuinoa Azam FC ili kurithi mikoba ya Mholanzi, Hans van der Pluijm aliyetimuliwa.

Hivi karibuni klabu ya Azam ilimfungashia virago Pluijm sambamba na msaidizi wake, Juma Mwambusi, kutokana na timu hiyo kupata matokeo mabaya katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza na BINGWA jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Abdulkarim Amin maarufu Popat, alisema mpaka sasa idadi ya makocha waliowasilisha wasifu wao wamefikia 10 huku akiwataja watatu kati ya hao.

Alisema miongoni mwa waliotuma maombi yao kuna makocha waliowahi kuzifundisha timu za Simba na Yanga akiwamo Goran Copunovic raia wa Serbia aliyekinoa kikosi cha Msimbazi msimu wa 2014 /15.

Pia alimtaja Basena aliyewahi kukinoa kikosi cha Simba msimu wa Ligi Kuu wa 2011/12 na mwingine ni Mbrazil aliyemtaja kwa jina moja la Renado, amewahi kuwa msaidizi wa Marcio Maximo.

“Makocha ni wengi na baadhi wamezifundisha timu za Simba na Yanga, lakini bado hatujachagua hata mmoja kati ya wote waliotuma wasifu wao,” alisema Popat.

Kwa sasa kikosi cha Azam kinanolewa na kocha mzawa aliyepewa kibarua hicho kwa muda, Idd Cheche.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*