AUSSEMS: UBINGWA UPO PALE PALE

WINFRIDA MTOI

SIMBA imeshindwa kutoka uwanjani na pointi zote tatu katika mchezo wao wa jana wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kutoka suluhu na Azam huku Kocha Mkuu wa Wekundu wa Msimbazi hao, Patrick Aussems, akitamba kuwa kiu yao ya kutwaa ubingwa ipo pale pale.

Jumapili iliyopita Simba ilipoteza pointi zote tatu katika mchezo mwingine wa ligi hiyo uliopigwa kwenye uwanja huo dhidi ya Kagera Sugar, walipofungwa bao 1-0 ikiwa ni siku chache baada ya kuichabanga Coastal Union mabao 8-1 dimbani hapo.

Kwa matokeo hayo ya jana, Simba iliyocheza michezo 33 imefikisha pointi 82, ikiendelea kukaa kileleni mwa ligi hiyo huku Azam waliocheza mechi 36 wakibaki nafasi ya tatu na pointi zao 69, wakati Yanga wakishika nafasi ya pili baada ya kujikusanyia pointi 80 kutokana na mechi 35.

Mchezo huo ulikuwa wa ushindani kuanzia mwanzo hadi mwisho ambapo Azam ndio waliokuwa wa kwanza kulifikia lango la Simba kupitia kwa beki wao, Bruce Kangwa ambaye dakika ya tisa alikosa bao baada ya kupiga mpira wa adhabu uliookolewa na kipa Aishi Manula.

Adhabu hiyo ilitokana na mshambuliaji wa Azam, Obrey Chirwa, kumfanyia madhambi beki wa kushoto wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ nje kidogo ya 18.

Dakika ya 13, Emmanuel Okwi wa Simba aliwatoka mabeki wa Azam na kuingia ndani ya boksi, lakini alipiga mpira uliookolewa na beki wa wakali hao wa Chamazi, Agrey Morris.

Mshambuliaji wa Azam, Joseph Mahundi, alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 20 kwa kumchezea vibaya kiungo wa Simba, Clatous Chama.

Mchezo huo uliendelea kwa kasi ambapo dakika ya 27, Meddie Kagere wa Simba alishindwa kufunga baada ya kupata krosi murua kutoka kwa Tshabalala kwa shuti lake kupanguliwa na kipa wa Azam, Razak Abalora.

Katika dakika 29, Donald Ngoma wa Azam, alikosa bao akiwa ndani ya 18 ambapo baada ya kupokea krosi ya Kangwa, alipiga shuti kali lililopaa.

Dakika mbili baadaye, Simba walijibu shambulizi hilo kupitia kwa Tshabalala aliyeachia shuti kali ambalo hata hivyo, lilikwenda pembeni ya goli.

Kiungo wa Simba, Haruna Niyonzima, alikaribia kuifungia timu yake bao dakika ya 43 pale alipopiga shuti kali akiwa karibu ya goli la Azam, lakini likaenda nje.

Dakika ya 59, Okwi alionyeshwa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi kipa wa Azam, Abarola na dakika mbili baadaye, Kangwa alionyeshwa kadi kama hiyo kwa kumchezea vibaya Kagere.

Baada ya kosa kosa hizo, timu zote mbili ziliendelea kushambuliana kusaka bao la kuongoza, huku shambulizi kali zaidi likiwa ni lile la dakika ya 73 lililofanywa na Simba, lakini halikuzaa matunda.

Niyonzima aliwahadaa mabeki wa Azam na kumchomekea Chama pasi maridadi, lakini Mzambia huyo alikosa bao baada ya shuti lake kupaa.

Baada ya mchezo huo, makocha wa timu zote mbili walipata nafasi ya kutoa tathmini zao, kila mmoja akisifia kiwango kilichoonyeshwa na pande zote mbili.

Kwa upande wake, Aussems alisema: “Mchezo ulikuwa ni mzuri, tunachoshukuru tumepata pointi moja. Lengo letu la kutwaa ubingwa lipo pale pale, tunajua lazima tutapata pointi sita katika mechi zetu zijazo dhidi ya Mtibwa Sugar na Ndanda ambazo zitatuwezesha kujiweka kwenye nafasi kubwa ya kubeba kombe.”

Alisema jana walijaribu kila aina ya mbinu walizonazo ili kupata mabao, lakini walishindwa akiwasifia Azam kwa kandanda safi walilolionyesha.

Naye Kocha wa Azam, Abdul Mingange, alisema kuwa walichokuwa wakitaka katika mchezo huo ni sare kwani walifahamu wapinzani wao ni wazuri, wakiwa wanausaka ubingwa kwa nguvu zote.

Katika hatua nyingine, kiungo mahiri wa Azam, Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr’, aliishia kuukodolea macho mchezo huo akiwa jukwaani kutokana na kutumikia kadi tatu za njano.

Kikosi cha Simba: Aishi Manula, Nicholas Gyan, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Yusuph Mlipili, Erasto Nyoni, James Kotei/John Bocco (dk 70), Haruna Niyonzima, Jonas Mkude, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na Clatous Chama.

Kikosi cha Azam: Razak Abarola, Nicholas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Morris, Stephen Kingwe, Joseph Mahundi, Frank Domayo, Obrey Chirwa, Donald Ngoma na Ramadhan Singano ‘Messi’/Daniel Lyanga (dk 53).


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*