AUSSEMS FANTASTIC

*Atinga Taifa usiku kama ninja

*Walinzi wapigwa butwaa, atamba AS Vita kwishnei

NA ZAITUNI KIBWANA

KAULIMBIU ya Simba ya kufa au kupona kuelekea mchezo wao wa kesho wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita ya DR Congo, imeonekana kumpandisha mzuka kocha wa timu hiyo, Patrick Auseems na kufanya tukio lililowashangaza wengi.

Simba itawakaribisha wageni wao hao katika mchezo huo wa Kundi D utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo mshindi atatinga robo fainali ya michuano hiyo ya Afrika.

Mbali ya timu hizo, nyingine zenye nafasi ya kusonga mbele kutoka kundi hilo ni mshindi kati ya Al Ahly ya Misri na JS Saoura ya Algeria zitakazopambana kesho jijini Cairo.

Katika msimamo wa kundi hilo, JS Saoura wapo kileleni wakiwa na pointi nane, Al Ahly wakifuatia na pointi zao saba sawa na AS Vita, huku Simba wakishika mkia na pointi zao sita, timu zote hizo zikiwa zimecheza mechi tano.

Hivyo timu itakayoshinda kati ya Simba na AS Vita, itaungana na mshindi kati ya Al Ahly na JS Saoura kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kutokana na jinsi walivyopania kuichapa AS Vita kesho na hivyo kutinga robo fainali, klabu ya Simba imekuja na kaulimbiu matata ya kufa au kupona, lengo likiwa ni kuwahamasisha wachezaji, viongozi na mashabiki kuungana kuhakikisha wanashinda kesho.

Kauli mbiu hiyo si tu imewagusa wachezaji na mashabiki wa Simba, bali pia kocha wao, Aussems.

Ili kutowaangusha waajiri wake hao katika kaulimbiu yao hiyo, Mbelgiji huyo juzi alipiga hesabu kali na kuja na jibu kwamba kwa kuwa mechi yao itaanza saa moja usiku, basi naye alihitaji kuwafua vijana wake kuanzia muda huo.

Hivyo juzi aliwashtukiza wachezaji wake na kuwapeleka Uwanja wa Taifa saa moja usiku tayari kuwapa mazoezi ‘bab kubwa’ ambayo yalilenga kuwazoesha kumudu kucheza muda huo bila wasiwasi wowote, wakitumia taa za uwanjani hapo.

Mara baada ya kufika kwenye uwanja huo, walinzi walipagawa wakishindwa kuamini kile kilichotokea, wakiishia kumkodolea macho Aussems na vijana wake wakiingia dimbani kufanya mambo yao.

Mbali ya wachezaji, makomandoo kadha wa kadha wa Simba, walikuwapo nje na ndani ya uwanja huo kuhakikisha hakuna yeyote atakayefika eneo hilo na kutibua plani zao.

Akizungumza na BINGWA jana, Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu, alisema wamelazimika kufanya mazoezi usiku kwa sababu mchezo wao utachezwa muda huo.

“Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeagiza michezo yote ya mwisho ichezwe muda mmoja, hivyo sisi mechi ni saa 1:00 usiku ndiyo sababu iliyotufanya tufanye mazoezi usiku,” alisema.

Kwa upande wake, Aussems, alisema kikosi chake kipo vizuri na tayari ameyafanyia kazi kasoro zilizojitokeza katika michezo iliyopita.

Alisema kikubwa anachokifanya ni kuhimiza vijana wake kuwa makini hasa katika safu ya ushambuliaji pamoja na mabeki, huku akisisitiza vijana wake kutofanya kosa lolote linaloweza kuwagharimu.

Katika hatua nyingine, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, amesema kuwa mgeni rasmi wa mchezo huo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, anayeshughulikia Muungano na Mazingira, January Makamba.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*