AS Vita walala kwa mafungu


MWAMVITA MTANDA

JAPO waliichapa Simba mabao 5-0 kwao jijini Kinshasa, timu ya AS Vita ya DR Congo, imeonekana kujawa na hofu na wapinzani wao hao watakaovaana nao leo, baada ya kujihami kwa wachezaji wake kulala mafungu mafungu.

Mchezo huo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo ambapo mshindi ataungana na mbabe baina ya Al Ahly ya Misri na JS Saoura ya Algeria kutinga robo fainali ya michuano hiyo.

Akizungumza na BINGWA jana, kocha msaidizi wa AS Vita, Raoul Shungu, alisema kuwa kutokana na uzito wa mechi hiyo, si vyema kutambulika mahali ambako timu yao imefikia kwa ajili ya usalama.

“Unajua hapa tuko ugenini, japokuwa naelewa Tanzania ni wakarimu, lakini tumekuja kimchezo na kila mmoja anahitaji ushindi, sasa tukianza kutangaza mahali tulipo, sio vyema chochote kinaweza kutokea.

“Jambo la msingi watu wanapaswa kutambua kwamba tupo hapa na tupo tayari kwa ajili ya mchezo huo, pia tumejipanga vizuri kupambana ili tuondoke na ushindi,” alisema Shungu.

Kwa mujibu wa chanzo cha ndani ya uongozi wa timu hiyo, awali uongozi wa AS Vita ulifikia katika Hoteli ya Peacock, iliyopo Mnazi Mmoja, Dar es Salaam na baadaye kuhamia Hoteli ya Kilimanjaro, jijini.

Aidha, mtoa habari wetu huyo alisema kuwa wachezaji na makocha walifikia katika Hoteli ya Souther Sun, iliyopo Oysterbay, jijini na viongozi wengine walifikia kwenye nyumba za watu binafsi.

Habari zaidi zinadai kuwa wachezaji wa timu hiyo pamoja na viongozi wao, walipanga kulala katika hoteli moja ambayo hata hivyo ilifanywa kuwa siri, baada ya mazoezi ya jana yaliyotarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Taifa.

“Tangu tupo Kongo tulipewa taarifa kuwa wenzetu wamejipanga kila idara ili kuhakikisha tunafungwa, hivyo tulipofika hapa, tunashukuru kuna watu wetu waliotangulia walipata ushirikiano wa kutosha, ikiwa ni pamoja na kuelekezwa nini cha kufanya ili kuepuka mbinu zozote za watu wa Simba zitakazolenga kutudhoofisha,” alisema mtoa habari wetu huyo.

Katika hatua nyingine, Shungu amewataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Taifa leo ili kuwapa sapoti akiahidi kutowaangusha. “Nafahamu mashabiki wa Yanga wanatamani tuifunge Simba kesho (leo), nawaomba waje kwa wingi uwanjani kutushangilia tutafanya kile wanachokitarajia,” alisema Shungu aliyewahi kuinoa timu hiyo ya Jangwani kwa mafanikio makubwa kati ya msimu wa mwaka 1999 hadi 2001 na kuipa ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati na Kombe la Nyerere. 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*