Ajib akusanya kijiji Dar

NA ZAITUNI KIBWANA

WAKATI Yanga ikishuka Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza leo kuvaana na African Lyon katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, nahodha wa timu hiyo, Ibrahim Ajib, amekuwa kivutio kwa wakazi wa Magomeni, jijini Dar es Salaam.

Ajib ameachwa Dar es Salaam kwa madai ya kutokuwa fiti kutokana na jeraha la nyonga linalomkabili na tayari ameanza kujifua kivyake ili kujiweka sawa kabla ya kurejea kundini.

BINGWA juzi lilimshuhudia nyota huyo akijifua kwenye Uwanja wa Barafu uliopo Magomeni, Dar es Salaam na kukusanya umati wa mashabiki waliokuwa wakimwangalia mkali huyo wa pasi za mabao (assist) akifanya yake.

Ajib ambaye kwa siku za karibuni anatajwa kuwaniwa na waajiri wake wa zamani, Simba, amekosa michezo miwili ya Yanga kutokana na kuuguza jeraha lake la nyonga.

Akizungumza na BINGWA kwenye uwanja huo wa Barafu juzi, mwanachama wa Yanga, mwenye kadi namba 873, Abrahmani Yassin, alisema kuwa Ajib ni mchezaji anayejielewa ndani ya kikosi hicho ndio maana aliamua kuacha kazi zake na kumwangalia akijifua.

“Tuna mechi nyingi mbele yetu, tunataka ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA (Kombe la Shirikisho la Azam), kurejea kwa Ajib kutatusaidia sana,” alisema.

Wakati Ajib akitoa uhondo kwa wakazi wa Magomeni, kumewahakikishia mashabiki wao pointi tatu dhidi ya African Lyon leo.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema anauchukulia kawaida mchezo huo sawa na mingine waliyocheza awali, akiweka wazi shauku yao ya kuvuna pointi zote tatu.

“Ni mchezo wa kawaida kama michezo mengine, tumejipanga kushinda, hakuna timu inayoingia uwanjani kwa mategemeo ya kushindwa,” alisema.

Kwa upande wake, kiungo wa timu hiyo, Said Juma Makapu, alisema kuwa wamejipanga kutoka uwanjani na ushindi hivyo mashabiki wao wasiwe na wasiwasi, waliopo Mwanza wafike kwa wingi CCM Kirumba na wale wa mikoani wasikae mbali na runinga zao.

Yanga ndio vinara wa Ligi Kuu Bara kwa sasa baada ya kukusanya pointi 68 katika michezo 29, Azam wakishika nafasi ya pili, huku mabingwa watetezi, Simba, wakisalia nafasi ya tatu na pointi zao 57 walizovuna kutokana na mechi 22 tu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*