… Tariq Seif aomba jezi ya Makambo

MWANDISHI WETU

BAADA ya taarifa za timu ya Horoya FC ya Guinea kumsajili nyota wa Yanga, Heritier Makambo, mshambuliaji wa Biashara United, Tariq Seif ‘Shamba Boy’, ameomba kupewa jezi hiyo ya nyota wa DR Congo.

Picha za Makambo zimeonekana kwenye mtandao wa klabu ya Horoya FC baada ya kusaini mkataba wa miaka mitatu ya kuichezea timu hiyo.

Habari hizo za Makambo zimepokewa kwa furaha na mshambuliaji wa zamani wa Trasit Camp na Stand United kwa sasa anakipiga Biashara Utd, Tarif, akisema Yanga hawana sababu ya kupoteza muda na mshambuliaji huyo, bali watafute wachezaji wengine wa kuvaa jezi hiyo ya mchezaji huyo wa DR Congo.

“Kama Makambo ameenda kutafuta riziki yake nchi nyingine, uongozi wa Yanga hauna jinsi bali kubariki uamuzi wa mchezaji huyo na kuangalia wachezaji wengine hapa nchini na kuendelea na mambo mengine,” alisema Tariq akizungumza na BINGWA.

“Tanzania kuna wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa, ambao wanaweza wakavaa jezi hiyo ya Makambo na kufanya makubwa,” aliongeza.

Akiulizwa kama anaweza kuvaa jezi ya Makambo, Tariq ambaye wiki iliyopita aliifungia Biashara Utd bao pekee dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, mjini Musoma, alisema kama wakimfuata atakuwa tayari na ana uhakika wa kuisaidia timu hiyo.

“Yanga ni timu kubwa lakini presha za Yanga na Simba nazijua, hivyo nina uwezo wa kuvaa jezi ya Makambo na kuwasaidia vizuri msimu ujao kama watanihitaji,” alisema Tariq ambaye ametupia mabao matatu mfululizo akianzia kwenye ushindi wa 3-0 dhidi ya Lipuli, kisha akaweka moja dhidi ya Yanga na juzi wakishinda 1-0 na kupachika bao la kufutia machozi katika kipigo cha 2-1 kutoka kwa Alliance.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*